Serikali imeshauriwa kuelekeza nguvu kubwa kwenye sekta za uchumi ambazo zinagusa watu wengi zaidi ili wananchi waweze kuguswa moja kwa moja na hatua kubwa ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati (Lower-Middle Income Economy).
Ushauri huo umetolewa na Profesa Honest Ngowi ambaye ni mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe katika mahojiano maalumu na TBC kuhusu Benki ya Dunia (WB) kuitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati.
Prof. Ngowi amesema kuwa ili Tanzania iweze kubaki hapa ilipo na kupiga hatua juu zaidi kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu lazima itilie mkazo katika sekta zilizoifikisha hapa ambazo ukuaji wake ni wa tarakimu mbili.
“Sekta ambazo zimetufikisha hapa ndio hizo hizo za kukazia.. sekta zinazokuwa kwa tarakimu mbili ni kama vile ujenzi, mawasiliano, uchukuzi, uhifadhi wa mizigo, sekta ya fedha,” ameeleza Prof. Ngowi.
Hata hivyo amesema ni lazima nguvu ielekezwe kwenye sekta ambazo zitasaidia watu wengi zaidi kuondokana na umasikini kwani ni kitu kimoja kuwa na uchumi wa kati na ni kitu kingine kuondokana na umasikini.
“Sekta ya kilimo (ufugaji, uvuvi) ni sekta ambayo ina watu wengi lakini ni sekta ambayo inakuwa taratibu sana (kwa tarakimu moja). Kwa hiyo pamoja na kuwekea mkazo sekta ambazo zimetufikisha hapa tusisahau hizi sekta ambazo zina watu wengi kwa sababu ndizo zitakazofanya wafaidi hichi tunachokiita kipato cha kati,” amefafanua mchumi huyo.
Prof. Ngowi amehitimisha kwa kusema kwamba licha ya kuwa Tanzania kufikia hatua hii kunaambatana na kukosa baadhi ya vitu kama misamaha ya madeni au mikopo yenye masharti nafuu, lakini amesisitiza kuwa nchi haiwezi kuendelea kwa kuvitegemea hivyo, na kwamba lazima ijitutumue na kujitegemea zaidi.