New MV Victoria yafanya safari ya majaribio

0
339

Meli ya MV Victoria ambayo kwa sasa inatambulika kama New MV Victoria – Hapa Kazi Tu, imefanya uzinduzi wa safari yake ya kwanza ya majaribio  kutoka mkoani Mwanza kwenda Bukoba mkoani Kagera baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Ukarabati wa meli hiyo ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 23, utasaidia kuboresha huduma za usafiri katika ziwa Victoria kati ya mikoa ya Mwanza na Kagera.

Meli hiyo inafanya safari ya majaribio ikiwa na tani mia moja za mizigo zilizosafirishwa bure kufuatia agizo la Rais John Magufuli la kutaka wakati wa majaribio ya kwenda Bukoba na kurudi Mwanza, mizigo ya  abiria isafirishwe bure.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari hiyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, -Humphrey Polepole amesema kuwa kukamilika kwa ukarabati wa meli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba utasaidia kukuza uchumi wa mikoa hiyo na ile ya ukanda wa ziwa.

Baadhi ya wananchi waliosafiri na meli hiyo ya New MV Victoria kutoka Mwanza kwenda Bukoba wameipongeza serikali kwa kuweka kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kutatua kero za wananchi ikiwemo usafiri katika ziwa Victoria.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini – MSCL, -Erick Hamisi amesema kuwa baada ya safari hiyo ya majaribio itakayochukua kati ya sita na saba, zitafanyika taratibu za mwisho katika kipindi cha takribani siku kumi 14 ili meli hiyo iaanze kufanya kazi rasmi.