Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amerejesha fomu ya kuwania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa urais Zanzibar.
Profesa Mbarawa alichukua fomu Juni 19, mwaka huu katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, akiwa mwanachama wa 10 kufanya hivyo.
Leo amerejesha fomu hizo katika ofisi hiyo na kupokewa na Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, Galous Nyimbo.
Profesa Mbarawa alipochukua fomu aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtanguliza Mwenyezi Mungu katika safari hiyo na kuwataka wamuombee jambo alilolianzisha likawe na baraka kwake.
Baada ya kurejesha fomu, alikishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusimamia vizuri mchakato huo wa kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar.
Mbali ya kuwa Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa amewahi kuhudumu katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika Serikali ya Rais John Magufuli.