Rais Magufuli aeleza sababu za kumtumbua Mrisho Gambo na wenzake, atoa onyo

0
691

Rais John Magufuli ameeleza kuwa ameamua kutengua uteuzi wa viongozi watatu wa Mkoa wa Arusha kutokana na kutoshirikiana, kusababisha migogoro na hivyo kuwacheleweshe maendeleo wananchi wa mkoa huo.

Kauli ya Rais Magufuli imekuja ikiwa ni siku mbili tangu alipotengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt Maulid Madeni kutokana na viongozi hao kutoelewana na kugombana bila sababu za msingi licha ya kuonywa mara kadhaa.

Rais ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam leo wakati akimuapisha Idd Kimanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, pamoja na viongozi wengine ambapoa amewataka kuhakikisha kuwa vitendo kama hivyo hivyo havijirudii kwa wateule wapya na viongozi wengine nchini.

Aidha, amemueagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jen John Mbungo kuwaonya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi kutokana na kufanya majukumu yasiyowahusu.

Pia, Rais Magufuli amewataka viongozi aliwaoteua kushika nyadhifa mbalimbali kutosheka na nafasi walizoteuliwa.