Tatizo la upatikanaji vitambulisho vya Taifa kuwa historia

0
205

Mitambo mipya kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa inatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni baada ya wataalam wa kuendesha mitambo hiyo kuwasili nchini kutoka nchini Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene amesema mitambo hiyo ambayo ni ya kisasa, ina uwezo wa kutengeneza vitambulisho laki moja na themanini elfu kwa siku.

Amesema mitambo hiyo iliishafungwa muda mrefu katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na ilipaswa iwe imeanza kufanya kazi mwezi Aprili mwaka huu, lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona ilichelewa kuanza kufanya kazi kutokana na watalaam wa mitambo hiyo kutoka Ujerumani kushindwa kuja nchini.

Akizungumza na wakazi wa kata ya na Ipela wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Waziri Simbachawene amewataka Wananchi wote ambao hawajapata vitambulisho vya Taifa kuondoa hofu, kwani kuanza kufanya kazi kwa mitambo hiyo kutawawezesha kupata vitambulisho hivyo kwa haraka.