Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Gaguti ametoa muda wa siku saba kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Biharamulo waliokusanya fedha na kushindwa kuzipeleka benki wawe wamezipeleka kabla hatua kali za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao.
Brigedia Gaguti ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilichokuwa na lengo la kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo miongoni mwa hoja hizo ni zaidi ya shilingi milioni 224 za makusanyo kutopelekwa benki.
Amesema licha ya halmashauri kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato na kupata hati safi, bado kuna watendaji wasio waaminifu ambao wamekuwa wakishindwa kusimamia mapato hayo.
“CAG ametoa hoja mbalimbali kuhusu halmashauri hii na nyingi zinalalia masuala ya fedha, natoa siku saba kwa watendaji ambao wamehusika na kutopelekwa fedha hizi wawe wamezirejesha mara moja na kwenye hili sitanii kabisa tutakuja kuonana wabaya kwenye fedha za umma,” amesisitiza Gaguti.
Amemuomba mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuitisha kikao kingine maalumu ambacho kitakuwa na agenda za kuangalia mwenendo mzima wa watumishi ndani ya halmashauri hiyo ili hatua husika ziweze kuchukuliwa pale itakapostahili.
“Mwenyekiti nataka kabla ya baraza hili kumaliza muda wake niitiwe kikao kingine mahususi kwa ajili ya madiwani pamoja na watumishi wote ili kuweza kuchukua hatua nyingine za kinidhamu kwa watumishi ambao wameonesha vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma lakini na mienendo mibaya,” amesema mkuu huyo wa mkoa.