Waziri Kairuki: Changamkieni fursa za uwekezaji wa mafuta ya alizeti

0
331

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki ametoa rai kwa Watanzania kuwekeza katika sekta ya mafuta ya kula kwa kuzingatia uhitaji na soko lililopo ndani na nje ya nchi.

Waziri Kairuki ametoa rai hiyo mkoani Dodoma alipotembelea na kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula cha Sunshine, kinachozalisha mafuta yanayotengenezwa kwa kutumia malighafi ya alizeti yanayoitwa Sunbelt kilichopo katika eneo la Zuzu.

Akiwa katika ziara hiyo iliyokua na lengo la kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za Wawekezaji nchini, Waziri Kairuki amepongeza uwekezaji katika kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 25 kwa siku na kilichowekeza zaidi ya shilingi bilioni 230.

“Niwapongeze kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya katika eneo hili tangu mwaka 2015, na hii inaleta chachu kwa wawekezaji wazawa kuona fursa na soko la malighafi wanazozalisha hasa zao la alizeti,”amesema Waziri Kairuki.

Amesema ni vema Watanzania wakaendelea kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la alizeti kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa mafuta ya kula nchini, kwani nchi imekuwa ikipoteza zaidi ya shilingi bilioni 443 kwa mwaka kwa kuagiza mafuta nje ya nchi.

Nae Meneja Biashara na Maendeleo wa kiwanda hicho cha kuzalisha mafuta ya kula cha Sunshine, Krishna Urs amesema changamoto inayowakabili ni uhaba wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji na ametoa wito kwa wadau kuitumia fursa ya kilimo cha zao hilo ili kuendana na mahitaji halisi.

“Ni muhimu kuwekeza zaidi katika alizeti kwa sababu soko lake lipo na hii itatatua changamoto ya kuzalisha kwa uchache na kuwafikia wananchi  wengi na kupata soko la nchi za nje”, amesema Krishna.