Hedhi: Hatua ya ukuaji iliyogeuzwa adhabu kwa mabinti

0
664

Kukosa pedi, maumivu wakati wa hedhi, baadhi ya dhana na imani potofu juu ya hedhi pamoja na kejeli kumepelekea baadhi ya mabinti kukosa ama kuacha shule.

Leo Mei 28, 2020 ni Siku ya Hedhi Duniani. Siku hii imetengwa maalum kwa ajili kuangalia umuhimu wa hedhi kwa wasichana na wanawake.

Kabla ya kufika mbali, tujikumbushe ‘hedhi’ ni nini hasa. Hedhi ni moja ya mabadiliko katika mwili wa msichana ambayo huiandaa nyumba ya uzazi kupata ujauzito. Mwanamke asipopata ujauzito baada ya maandalizi hayo damu humtoka ukeni ambayo ndiyo hedhi. Mzunguko huu huanza mara binti anakapovunja ungo na hutokea mara moja kila mwezi.

Kwa muda mrefu katika jamii zetu tumekuwa tukitafuta tafsida mbalimbali kuficha mambo yanayohusiana na hedhi. Yapo maeneo ambayo huita pedi mkate wa dada, huku kupata hedhi kukiitwa kunyesha hii ni mifano tu ya namna ambayo jamii nyingi za kiafrika zinavyochukulia jambo hili ambalo ni muhimu katika hatua za ukuaji wa mwanamke.

Mzunguko wa hedhi hutofautiana kati ya wanawake, wapo wenye mzunguko wa siku 28 na wengine hadi 30 lakini pia wapo wengine wenye mizunguko mirefu zaidi, wengine mizunguko yao ni mifupi na wengine wenye mizunguko inayobadilika badilika, na hapo ndipo unaposhauriwa kuonana na mtaalamu wa afya.

Kukosa siku zako ama kuwa na mzunguko unaobadilika badilika huweza kuathiri afya ya uzazi. Hali hii huweza kusababishwa na mambo mbalimbali yakiwemo matumizi ya dawa, msongo wa mawazo, matatizo ya kiafya na mambo mengine mengi.

Ni vyema kuendelea kutoa elimu ya hedhi kwa watoto, mabinti na vijana ili kuweza kuondoa dhana potofu zinazohusishwa na hedhi.

Ni muhimu kufuatilia usafi wa mara kwa mara uwapo kwenye hedhi ili kujiepusha na magonjwa kama ‘Toxic Shock Syndrome’ unaosababishwa na kutobadilisha taulo za kike (pedi) kwa muda mrefu.

Picha: DW