Mfumo wa stakabadhi ghalani kutumika katika uuzaji ufuta

0
457

Mkoa wa Pwani umeanza  utaratibu mpya wa uuzaji wa zao la ufuta kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani, ili kudhibiti udanganyifu unaofanywa wakulima wa kuchanganya zao hilo na mchanga.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evaristi Ndikilo amesema  utaratibu huo utaanza kutumika mwishoni mwa mwezi June mwaka huu wakati msimu mpya wa ununuzi wa zao la ufuta utakapoanza.

Amesema lengo la kuanza kutumia utaratibu mpya wa uuzaji wa zao la ufuta kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ni kuhakikisha zao la ufuta linawanufaisha wakulima wa mkoa wa Pwani  pamoja na kuchangia  pato la Taifa.

Kupitia utaratibu huo minada yote ya zao la  ufuta itakuwa ikifanywa kwa njia ya Kielekroniki chini ya usimamizi wa soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania,- Augustino Mbulimi amesema uuzaji wa mazao kwa kutuma mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani unamanufaa makubwa kwa wakulima  tofauti na mifumo inayotumika hivi sasa.

Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021, mkoa wa Pwani unatarajia kuvuna zaidi ya tani elfu 13 za ufuta.