Corona: Afrika Kusini yaruhusu kufunguliwa kwa nyumba za ibada

0
774

Ikiwa ni muendelezo wa nchi mbalimbali duniani kuelegeza masharti zilizoweka kwa ajili ya kudhibiti virusi vya corona, Afrika Kusini imeruhusu kufunguliwa kwa nyumba za ibada kuanzia Juni 2020.

Akitangaza uamuzi huo, Rais Cyril Ramaphosa amesema kuwa licha ya ruhusa hiyo, nyumba hizo hazitoruhusiwa kuwepo watu zaidi ya 50 kwa wakati mmoja.

Aidha, Ramaphosa amesema ni lazima umbali kati ya muumini mmoja na mwingine uzingatiwe na wavae barakoa wakati wote, huku akisema shughuli zote za ibada ambazo zinaweza kusababisha maambukizi ya corona ziepukwe.

Afrika Kusini ilifungwa tangu mwishoni mwa Machi mwaka huu serikali ilipochukua hatua kadhaa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo ambavyo tayari vimeathiri watu 23,615 na kusababisha vifo 481 nchini humo.

Kutokana na marufuku kadhaa, nyumba za ibada zilibadili mfumo wa utoaji huduma na kuanza kutumia redio, runinga na intaneti kwa wingi ili watu waweze kufuatia wakiwa majumbani.

Nchi hiyo itaingia katika hatua ya tatu kati ya hatua tano za lockdown ilizoweka, ambapo katika hatua hiyo shughuli mbalimbali za kiuchumi zitarejea.