BoT yatoa muongozo wa utendaji kwa watoa huduma ndogo za fedha

0
395

Benki Kuu ya Tanzania imesema imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha nchini yakiwemo kutokupewa mikataba ya mikopo, kutokupewa taarifa ya mikopo (loan statement) wanapotakakulipa mikopo hiyo.

Malalamiko mengine ni kuchelewa kujibiwa maombi yao ya kulipa mkopo mapema na kutozwa riba na gharama zingine kubwa wanapotaka kulipa mkopo mapema.

Kutokana na malalamiko hayo, BoT imewaagiza watoa huduma hao wanaolalamikiwa kuchukuwa hatua zifuatazo:

Kwanza, kuweka mfumo wa kutatua malalamiko ya wateja kwa mujibu wa Kanuni ya 54 ya Kanuni za Watoa Huduma Ndogo za Fedha (Wasio Pokea Amana) za Mwaka 2019, katika kipindi cha wiki 2.

Pili, kukusanya na kuwasilisha BoT taarifa za malalamiko yote zikionesha jina la mlalamikaji, namba ya simu ya mlalamikaji, makazi ya mlakamikaji (Mkoa, Wilaya na Tawi husika), kiasi cha mkopo husika, tarehe ya kukopa, riba, tozo mbalimbali, kiasi cha rejesho (installment), kiasi kilicholipwa mpaka muda huo, muda wa kuiva kwa mkopo; kiini cha malalamiko, tarehe ya kupokea lalamiko na hatua zinazochukuliwa na kampuni husika.

Tatu, kutatua malalamikotajwa katika kipindi cha wiki tatu na malalamiko yaliyoshindikana yawasilishwe benki kuu pamoja na sababu za kushindwa kutatuliwa.

Nne, kuzingatia matakwa yote ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 iliyoanza kutumika tarehe 1 Novemba 2019 wakati wakiendelea na mchakato wa kuomba Leseni Benki Kuu.

Aidha, benki kuu imesema itachukuwa hatua za kisheria, ikiwemo kuwafungia biashara watoa huduma ndogo za fedha watakaokaidi maelekezo yaliyotolewa.