Waziri wa afya awatoa hofu Watanzania kuhusu kutokuwepo taarifa za corona

0
947

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kwa siku za hivi karibu serikali haijatoa taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini kwa sababu ya maaabara ya taifa ipo katika matengenezo.

Ummy Mwalimu akizindua mfumo wa mawasiliano wa huduma kwa wateja katika wizara hiyo amesema maabara ikikamilika taarifa zitatolewa.

Hata hivyo amewasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari pamoja na kufuata maelezo ya wataalam ya kujikinga na virusi vya corona, na kwamba serikali kutokutoa taarifa isiaminike kuwa ugonjwa huo haupo.

“Wakati hatutoi taarifa za maabara, nitumie fursa hii kuwataka wananchi kuzingatia kuwa ugonjwa wa corona bado upo, waendelea kujikinga kama tunavyoeleza mara kwa mara,” amesema kiongozi huyo.

Akirudi kauli ambayo imekuwa ikisisitizwa na Rais John Magufuli, Waziri Ummy amewataka Watanzania kutokuwa na hofu, badala yake wachukue tahadhari kama wafanyavyo kwa magonjwa mengine ya kuambukiza.