Vuguvugu la mivutano likiendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mbunge wa Momba ameibuka na kutangaza kujiuzulu nafasi za uongozi ndani ya chama.
David Silinde ametangaza hilo bungeni mjini Dodoma ambapo ameeleza kuwa tayari amemuandikia barua mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, John Mnyika kuhusu uamuzi wa kujiuzulu.
“Nimemuandikia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na katibu mkuu kuwa nimejiuzulu nafasi yangu ya Katibu wa Wabunge na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Viwanda na Biashara,” amesema Shilinde.
Uamuzi huo umekuja baada ya kushinikizwa na wabunge wengine wa chama hicho kutokana na kutotii agizo lililotolewa na Mbowe la kuwataka wabunge wote kutohudhuria vikao vya bunge.
Silinde amesema kuwa waliompeleka bungeni ni wananchi na kwamba chama ni mdhamini tu, hivyo hata kama atakosa udhamini wa CHADEMA, wananchi wanaweza kuamua kumchagua kwa chama kingine.
Wakati hilo likitokea, wabunge wa chama hicho pia wamemtaka Mbunge wa viti maalum Maryam Msabaha kujiuzulu nafasi yake ya ujumbe wa kamati kuu kwa kushindwa kufuata makubaliano ya wabunge na maelekezo ya chama.