Kamati yaundwa kuichunguza Maabara ya Taifa

0
236

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amemuelekeza katibu mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia afya kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ili kupisha uchunguzi.

Ummy Mwalimu ametoa agizo hilo ikiwa ni siku moja tangu Rais wa Tanzania, John Magufuli alipobainisha changamoto za kiutendaji katika taasisi hiyo, hasa katika upimaji na utoaji majibu wa sampuli za virusi vya corona.

Katika taarifa ya wizara hiyo, Waziri Ummy ameelekeza kusimamishwa kazi mkurugenzi wa maabara hiyo, Dkt. Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora, Jacob Lusekelo.

Aidha, waziri ameunda kamati ya wabobezi 10 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa maabara hiyo, ikiwemo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za COVID-19.

Kamati hiyo itakayoongozwa na Prof. Eligius Lyamuya inaanza kazi mara moja na itatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa waziri wa afya Mei 13, 2020.

Sambamba na uchunguzi utakaokuwa ukifanyika, shughuli za upimaji wa sampuli katika maabara zitaendelea.