Kampuni ya ATCL yaanza kusafirisha mizigo nje ya nchi

0
1456

Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imeanza rasmi safari ya kusafirisha mizigo kwenda nje ya nchi, ikiwa ni moja ya mikakati ya kampuni hiyo kujiimarisha kibiashara katika kipindi hichi cha corona.

Kampuni hiyo ambayo imeathiriwa kwa kupungua kwa abiria na baadhi ya nchi kuzuia ndege kuingia, imesema imeanza kutumia ndege zake kusafirisha mizigo hiyo ambapo leo ndege ya kwanza imepeleka mazao ya vyakula nchini Comoro.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Innocent Swai ambaye ni Afisa Mauzo na Mizigo wa Kampuni ya ATCL ameeleza kuwa kutokana na nchi nyingi kufunga mipaka na kuzuia abiria, imewalazimu wao kuangalia fursa nyingine.

“Moja wapo ya fursa tuliyoiona ni mizigo, na mizigo inayopelekwa Comoro ni mazao ya vyakula,” ameeleza Afisa huyo.

Aidha, ameongeza kuwa “Siyo kwamba tutaenda Comoro tu, tulikuwa na ndege yetu kubwa, Dreamliner, iliyokuwa ikienda India mara tatu kwa wiki, hivyo kuanzia wiki wa pili ya mwezi wa tano tutaanza kupeleka mizigo India.”

Shirika hilo limesema kuwa pia litafanya safari za kupeleka vyakula vya baharini Guangzhou nchini China.

Hadi sasa kampuni hiyo ina ndege nane zilizonunuliwa hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali kulifufua, na kuhakikisha linakuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa taifa.