Bilioni 9.5 yaongezeka bajeti ya Wizara ya Habari 2020/2021

0
475
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma ambapo ameomba kutengewa kiasi cha TZS bilioni 40.1 kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imeongezeka hadi kufikia kiasi cha TZS bilioni 40.1 kutoka TZS Bilioni 30.9 kwa mwaka wa fedha uliopita ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema ongezeko la TZS bilioni 9.2 litaenda kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Katika mwaka wa fedha ujao fedha zitaenda kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika yenye kiasi cha TZS milioni 515, Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kilichotengewa TZS milioni 250 kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kiasi cha TZS milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni pamoja na viwanja vya michezo,” amesema Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa eneo Changamani la michezo Dar es Salaam na Dodoma ambao umetengewa kiasi cha TZS milioni 650, mradi wa upanuzi wa usikivu redio za TBC Taifa na TBC FM ambao umetengewa kiasi cha TZS bilioni 5 pamoja na mradi wa Habari kwa Umma ambao umetengewa kiasi cha TZS bilioni 1 inayofanya miradi yote kutekelezwa kwa jumla ya TZS bilioni 7.7.

Akizungumzia sekta ya michezo, amesema kuwa ni sekta ambayo inaimarisha afya na kulitangaza Taifa ndio maana leo nchi inasikika katika matangazo ya Premier League na UEFA kupitia vijana wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi akiwemo Mbwana Samatta pia mafanikio ya timu ya wanawake ya mpira wa miguu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali imefanya mambo makubwa kwa sekta za Wizara hiyo muhimu kwa nchi, na fedha zilizopitishwa zitaenda kuboresha mkakati wa kuitangaza lugha ya Kiswahili ambayo ni bidhaa adhimu duniani kwa kuwekeza kununua vifaa vya ukalimani, kufundisha wakalimani, kutengeneza vitabu ambavyo vitakuwa ni miongozo ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni.

“Kwa mara ya kwanza tumepata bajeti kwa ajili ya taasisi yetu ambayo ni Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambayo kwa miaka mingi ilikuwa inajitegemea na kujiendesha kibiashara lakini kwa sasa Serikali imefanya uamuzi TSN watalipwa mishahara na Serikali ili waweze kuwekeza katika maeneo mengine”, alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua kuwa mafanikio yaliyopo katika wizara hiyo yametokana na ushirikiano ambao inaupata kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari na wanahabari, wasanii, wanautamaduni na wanamichezo wote nchini.

Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Amina amesema kuwa usimamizi mzuri na utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo umefanya sekta zake zifanye vizuri ikiwemo sekta ya habari ambayo tofauti na nchi nyingi duniani, Tanzania ina jumla ya televisheni zilizosajiliwa 44 pamoja na vituo vya redio 186.

Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 960,000,000 kupitia Idara ya Habari – MAELEZO na Maendeleo ya Michezo. Kwa upande wa taasisi saba zilizo chini ya wizara, kiasi kinachokadiriwa kukusanywa ni jumla ya shilingi bilioni 40.2.