Muhimbili yasambaza vazi maalumu kwa watoa huduma wa COVID-19

0
593

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kusambaza mavazi maalum (coverall) ambayo ni sehemu ya mavazi ya watoa huduma (PPE) kuvaa ili kujikinga wakati wanatoa huduma kwa wagonjwa wenye maambuki mbalimbali ikiwemo virusi vya corona.

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MNH, Zuhura Mawona amesema baada ya kujadiliana na serikali bei elekezi itakuwa shilingi 50,000 kwa kila vazi moja.

Manispaa ya Kinondoni imenunua mavazi 15 yenye thamani ya shilingi 750,000, Ilala mavazi 20 yenye thamani ya shilingi 1,000,000 huku Manispaa nyingine zikiendelea kulipia ili kupata mavazi hayo.

“Kwa sasa tunaanza na vituo vilivyopo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam, na mikoa mingine itafuata,” amesema Mawona

Amesema kuwa mahitaji ni makubwa katika mikoa mbalimbali hivyo kwa sasa muhimbili imejikita katika kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji.

Mapema wiki iliyopita muhimbili ilizindua vazi hilo maalumu liloshonwa na wataalamu wa hospitali hiyo kwa kutumia malighafi za ndani ya nchi lengo ikiwa ni kukabiliana na upungufu wa bidhaa hizo duniani.