Operesheni za TAKUKURU Kigoma zaokoa milioni 67

0
467
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Nestory Gatahwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hiyo mkoani humo.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kuokoa fedha kiasi cha shilingi milioni 67.5 katika kipindi cha Januari hadi Machi 2020 kutokana na opereshi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hiyo mkoani Kigoma, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Nestory Gatahwa amesema operesheni hizo zimehusisha Chama cha Ushirika cha RUMAKO kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Chuo cha Uganga Maweni pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.

Akitoa mchanganuo wa fedha hizo, Gatahwa amesema kiasi cha shilingi milioni 48.6 kimeokolewa katika Chama cha Msingi cha RUMAKO baada ya kufanyiwa ubadhilifu na viongozi wa chama hicho kwa kujikopesha bila kuzirejesha pamoja na manunuzi ya pembejeo hewa

Pia, kiasi cha Shilingi milioni 3.1 kimeokolewa kutoka fedha za ada zilizolipwa na wananchi katika Chuo cha Uganga Maweni kwa ajili ya kupata mafunzo ya usimamizi wa maduka ya dawa tangu mwaka 2015 bila kupata mafunzo hayo. Fedha hizo zimeokolewa na kurejeshwa kwa wananchi waliokuwa wanazidai.

Aidha, TAKUKURU imeweza kuokoa shilingi milioni 14.2 katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ambapo imesitisha malipo yaliyokuwa yameandaliwa kulipa kazi ambazo hazijafanyika.

Kiasi kingine cha shilingi milioni 1.5 kimeokolewa kutoka katika kazi za uchaguzi zilizohusisha idara ya uhamiaji na maliasili.