Na Frank Mvungi- MAELEZO Kigoma
Shilingi Bilioni 18.62 zilivyowezesha mageuzi ya miundombinu ya barabara za lami katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Manispaa hiyo Injinia Wilfred Shimba amesema kuwa barabara zilizojengwa zina urefu wa Kilomita 12 na ujenzi huo umehusisha njia za waenda kwa miguu, mifereji ya maji na taa za barabarani.
“Awali Manispaa ya Kigoma Ujiji ilikuwa na barabara moja tu yenye lami na kwa sasa kujengwa kwa barabara hizi kunachangia kukuza shughuli za kiuchumi na hivyo hata mapato yanaongezeka na mandhari ya mji inavutia zaidi kwa sasa,” amesisitiza Mhandisi Shimba
Akifafanua Mhandisi Shimba amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za Manispaa hiyo umekuwa chachu ya maendeleo katika Manispaa hiyo na imevutia na kuchangia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Amezitaja faida za mradi huo kuwa ni pamoja na; kurahisisha usafiri na usafirishaji ndani ya Manispaa hiyo, kuvutia uwekezaji, kufanya Manispaa hiyo kuwa na muonekano bora zaidi ya ilivyokuwa awali kabla ya kuboreshwa kwa miundombinu hiyo ikiwemo kuwekwa kwa taa za kuongozea magari.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo umekamilika na kuanza kuleta manufaa kwa wakazi wa Kigoma na wawekezaji wote wanaofika katika Manispaa hiyo kwa lengo la kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuchangia katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.
Kwa sasa baada ya kukamilika kwa kazi zote ambazo zipo katika mkataba wa ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, imeleta tija katika sehemu zote za maeneo ya mradi, hususani mfereji wa maji yam vu wa Katonyanga na barabara zote ili kupunguza adha za maji ya mvua kwa wakazi wa maeneo yote ya Manispaa ya Kigoma.
Kwa upande wake mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Bw. Yasin Ally amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi kwa makubwa katika ujenzi wa miundombinu ya Manispaa hiyo zikiwemo barabara za lami, taa na huduma za jamii zimeimarishwa.
Ameongeza kuwa kuimarishwa kwa miundombinu ni chachu ya maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo kwa ujumla.
Ujenzi wa barabara za lami katika Manispaa ya Kigoma Ujiji umefanyika katika mitaa ya Kaaya hadi Simu, Mwanga Kitabwe Mwembetogwa, Wafipa Kagera, Kagashe Road, Kukolwa Road, Ujenzi Nazareth, Maweni Burega.