Mahakama yataifisha bilioni 16 kuwa mali ya serikali

0
411

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama Mahakama ya Ufisadi imetaifisha zaidi shilingi bilioni 16 za upatu kuwa mali ya serikali.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga kuwasilisha maombi mahakamani hapo kuomba fedha hizo zitaifishwe kwa kuwa washtakiwa katika kesi hiyo hawajawahi kufika mahakamani.

Jaji wa mahakama hiyo, Elinaza Luvanda ametoa uamuzi huo baada ya kujiridhisha na vielelezo vilivyowasilishwa na DPP dhidi ya washtakiwa hao.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Huebenthal raia wa Ujerumani, na Frankricket raia wa Uingereza.

Februari 11, 2019, DPP aliwafungulia mashtaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam lakini hawajawahi kuripoti.

Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanadaiwa kuja nchini na kuanzisha Kampuni ya IMS Marketing Tanzania Limited, Novemba 19, 2014 na kupewa usajili wa namba 113133, ambapo baadaye walianza kuendesha upatu kinyume na sheria.

Katika kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kuanza kusaini nyaraka mbalimbali kwa mawakili kwa ajili ya hiyo kampuni, ambapo Aprili 23, 2015 walifungua akaunti mbili za dola za Marekani katika Benki ya Afrika (BOA), Tawi la NDC jijini Dar es Salaam kwa jina la Kampuni ya IMS.

Aidha, baada ya kutaifishwa kwa fedha hizo Jaji Luvanda aliyesikiliza shauri hilo, amekataa ombi la DPP la kutaka mahakama itoe amri ya kuamrisha Benki ya BOA kulipa riba ya kipindi chote walichohifadhi fedha hizo.