Waziri wa Afya, amesema kuwa leo pia hakuna kisa chochote cha mtu aliyethibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, na kwamba mgonjwa aliyekuwa na maambukizi ya virusi hivyo mkoani Kagera amepona.
Kutokana na hatua hiyo, Ummy Mwalimu amesema idadi ya watu waliopona ugonjwa wa homa ya mapafu nchini hadi sasa imefikia watatu, baada ya wawili kuwa tayari wametangazwa kupona.
“Na leo pia hatuna case [kisa] mpya za COVID19. Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3. Mgonjwa ali[y]ebaki wa Arusha vipimo vyake siku ya 9 leo ni Negative [hana maambukizi]. Tutampima siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona,” ameandika waziri kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Waziri Ummy ameongeza kuwa waathirika wengine 15 waliobaki wanaendelea vizuri na matibabu.
Aidha, amewashukuru wananchi kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga, kama vile kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, huku akiwasihi kuongeze nguvu katika kuepuka misongamano/mikusanyiko, pamoja na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.