Wizara ya Afya kupitia Idara kuu ya maendeleo ya Jamii imeanza kutoa mafunzo kwa Wataalamu wa Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuelimisha Jamii kuhusu ugonjwa unaoenezwa na Virusi vya Corona.
Akifungua mafunzo hayo kwa maafisa wa Wilaya na kata zote za Mkoa wa Arusha jijini Arusha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Hargeney Chitukuro amewataka kutumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kwa usahihi kuhusu maambukizi na namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona bila hofu.
Chitukuro amesema kuwa, tangu ugonjwa huo ulipoingia Mkoani Arusha, mafunzo mbalimbali yameshatolewa kwa wataalamu wa afya 240 na kuwaelekeza namna ya kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga.
Amewaomba pia wadau wote kuelekeza nguvu zao kushirikiana na Serikali katika kufanikisha ukarabati wa kituo cha dharura mkoani humo pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kujikinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike ametoa wito kwa Maafisa hao ili kuepusha msongamano watumie Redio za Jamii zilizopo kwenye maeneo yao kuelimisha jamii.