Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli ametoa wito kwa taasisi, mashirika, kampuni wafanyabiashara na watu wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji.
Mama magufuli ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akikabidhi msaada kwa vituo vya kulea watoto wenye mahitaji maalumu vya Cheshire Home na Nyumba ya Matumaini katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma.
Msaada huo umekabidhiwa kwa wawakilishi wachache wa watoto hao walioongozana na baadhi ya walezi wao, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima kutokana mlipuko wa virusi vya corona.
Akikabidhi msaada huo Mama Magufuli amesema kuwa, hiki ni kipindi cha Kwaresma ambapo waumini wa dini ya Kikristo wanahimizwa kufunga, kuomba na pia kujitoa kwa wenzao wenye uhitaji.
“Kwa kuzingatia hilo nami leo nimewaita hapa ili kutoa kazawadi kangu
kadogo kwa wanangu hawa”, amesema Mama Magufuli.
Msaada aliotoa Mama Magufuli kwa vituo hivyo vya kulea watoto wenye mahitaji maalumu vya Cheshire Home na Nyumba ya Matumaini ni pamoja na mchele tani mbili, unga wa sembe tani mbili, maharage kilo 830, mafuta ya kupika lita 830, sukari pamoja na vinywaji vya aina mbalimbali.