Korea Kusini yawasisitiza Watanzania kujilinda na corona

0
402

Balozi wa Korea Kusini nchini Cho, Tae-ick amewashauri Watanzania kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Balozi Tae-ick amesema kuwa kitu muhimu kwa sasa ni kumtambua mtu aliyeambukizwa virusi vya corona na kumtibu haraka ili asiwaambukize wengine.

Ameipongeza wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu virusi vya corona, hatua inayoonyesha utayari wa serikali katika kupambana na virusi hivyo.

Balozi huyo wa Korea Kusini nchini pia amezungumzia umuhimu wa kuendelezwa kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili katika sekta mbalimbali hasa Teknolojia.

Katika mahojiano hayo Balozi Tae-ick ameipongeza Tanzania kwa kuendeleza maeneo ya utalii pamoja na utamaduni wa Mtanzania, na kuongeza kuwa mambo hayo ni urithi mzuri.

“Wakorea wanapenda kuja kutalii Tanzania kwa sababu ya utajiri uliopo, lakini pia lugha ya Kiswahili ni kubwa na karimu, napenda maneno yanayoandikwa kwenye kanga na methali za kiswahili zina hekima, pia napenda kusoma magazeti ya Tanzania na kutazama Tanzania Safari Channel, vilevile tunajenga media center Serengeti”, amesema Balozi Tae-ick.