Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko mikubwa ya ndani ama ya hadhara kuanzia leo, ili kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na virusi vya corona.
Hatua hiyo imetangazwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)- Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Polepole amesema kuwa vikao vyote vya CCM ambavyo vipo kwenye kalenda vitaendelea kama ilivyopangwa kwa kuwa havihusishi idadi kubwa ya watu.
Ameviomba vyama vingine vya siasa nchini navyo kuchukua uamuzi kama uliochukuliwa na CCM, kwa kuwa mapambano dhidi ya virusi vya corona ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.
CCM imewataka Watanzania wote kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, yanayoelekeza namna ya kujikinga na virusi hivyo vya corona.
Pia CCM imeipongeza serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na virusi hivyo, na kuiomba kuendelea kuchukua hatua za dharura na za haraka za kukabiliana na corona.