Mambosasa awaonya wanaovunja sheria

0
164

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limetoa onyo kwa wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa pamoja na vikundi ambavyo vinatumia itikadi zao na kuvunja sheria za nchi na kusababisha usumbufu usio wa lazima.

Onyo hilo limetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Lazaro Mambosasa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kuongeza kuwa watu wa aina hiyo wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kuwa wanachokifanya ni kuhatarisha hali ya usalama.

Kamanda Mambosasa alikua akitoa ufafanuzi kuhusu kukamatwa kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Dar es salaam, wakati wakimpokea Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe wakati akitoka katika gereza la Segerea.

Machi Kumi mwaka huu, mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam iliwahukumu viongozi waandamizi wa CHADEMA pamoja na aliyekua Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt Vicent Mashinji kulipa faini ya jumla ya shilingi milioni 350 au kifungo cha miezi mitano kwa kila kosa baada ya kuwakuta na hatia ya makosa kumi na mawili.

Viongozi hao walilipa faini hiyo na kutoka gerezani.