Taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu wasafiri walioingia nchini kupitia KIA

0
291

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto amesema kuwa raia sita wa Norway na Denmark walioingia nchini Machi 13 mwaka huu wakitokea Kenya hawana maambukizi ya virusi vya Corona.

Kupitia taarifa kwa umma Ummy Mwalimu ameeleza kuwa raia hao walioingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) walikaguliwa joto la mwili na iligundulika kuwa mmoja ana homa ya nyuzi joto 38, pamoja na kihokohozi na mwili wake kuchoka.

Wasafiri hao walitengwa kwa kupelekwa eneo maalumu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, na wote walichukuliwa sampuli ambazo baada ya uchunguzi imebainika kuwa wapo salama, na wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

Kuhusu msafiri aliyekutwa na joto kali, Waziri Mwalimu amesema alikuwa na mafua ya kawaida.

Waziri amewatoa hofu wananchi kwamba hadi sasa Tanzania hakuna mtu mwenye maambuziki ya virusi hivyo, huku akiwataka kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga. Pia, amewahimiza wananchi kuto sambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na serikali.