Tanzania yaukosha Umoja wa Mataifa kupambana na dawa za kulevya

0
202

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kupitia kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, limeipongeza Tanzania kwa kuwa na jitihada madhubuti za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

Pongezi hizo za UNODC zimetolewa jijini Dar es salaam na Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini James Kaji wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, mkutano uliokua na lengo la kuelezea mafanikio yaliyopatikana nchini katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Amesema jitihada hizo zimeleta matokeo chanya katika mapambano ya dawa za kulevya duniani katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2020.

“Katika mkutano wa 63 wa Kamisheni ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (CND 63) uliofanyika nchini Austria, Mkuu wa shirika la UNODC alitupongeza Tanzania kuwa ni moja kati ya nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kupunguza upatikanaji na uhitaji wa dawa za kulevya, na kuweza kutekeleza mikakati minne ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwa uwiano ulio sawa” amesema Kaimu Kamishna Jenerali huyo wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.

Aidha amewataka waandishi wa habari kutoa taarifa za uhakika juu ya takwimu za kupambana na kudhibiti dawa za kulevya  nchini, kwani kwa kutoa takwimu za uongo kutasabisha hofu na taharuki katika jamii na kuchafua taswira ya  Tanzania.

“Pamoja na mafanikio hayo makubwa, bado tuna masikitiko makubwa kwa baadhi ya magazeti wanaichafua nchi yetu kwa kuandika habari zisizo sahihi kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya,  niwaombe kuwa makini katika uandishi wa habari na ni vyema kutumia vyanzo vya uhakika na kuzingatia maadili ya Uandishi” amesema Kamishna Kaji.