Bunge dogo la Russia limepitisha muswada unaoridhia kumuongezea muda wa kukaa madarakani Rais wa sasa wa nchi hiyo Vladimir Putin, ambaye muda wake wa uongozi unatarajiwa kumalizika ifikapo mwaka 2024.
Bunge hilo la Russia maarufu kama Duma, limeridhia Putin kuendelea kukaa madarakani kwa miaka mingine sita baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.
Hata hivyo uamuzi huo wa bunge la Duma utapaswa kupata ridhaa ya wananchi wa Russia.
Wananchi wa Russia watapiga kura ya maoni ama wakubali au wakatae mapendekezo hayo baadaye mwaka huu.
Putin ameliongoza Taifa la hilo kwa vipindi tofauti kama Rais, na kuna wakati aliwahi kuwa waziri mkuu, na baadaye kurejea tena madarakani akiwa kama Rais, nafasi anayoishikilia mpaka sasa.
Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Russia imepiga marufuku kampeni zote za kisiasa kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona hadi mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ingawa wachunguzi wa masuala ya siasa za nchi hiyo wanasema kuwa corona si tishio nchini humo bali tishio ni upinzani wa kisiasa.