Bilioni 15 zatolewa kumalizia ujenzi wa hospitali Mara

0
255

Rais John Magufuli ametoa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo mkoani Mara, ambayo imekua ikijengwa kwa muda wa miaka arobaini bila kumalizika.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, ziara iliyokua na lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea ujenzi huo Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, itakapokamilika hospitali hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa Wakazi wa mkoa wa Mara hasa kwa huduma za matibabu ya kibingwa.

“Kutakuwa hakuna haja ya kwenda hospitali ya Kanda Bugando kupata matibabu ya kibingwa kwani tunataka huduma za kibingwa zitolewe hapa hapa,” amesema Waziri huyo wa Afya

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Chuo Kikuu Ardhi kimepewa kazi ya kusimamia ujenzi wa hospitali hiyo, hivyo ameagiza kazi kufanyika usiku na mchana ili ujenzi huo umalizike katika muda uliopangwa.

Mkuu wa mkoa wa Mara, -Adam Malima amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa hospitali hiyo ya rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

“Hospitali hii imechukua awamu tano za Marais kumalizika, na tunamshukuru Rais kwa kuchukulia kipaumbele katika hili,” amesema Malima.