Zanzibar yawakaribisha wawekezaji kutoka Nigeria

0
1904

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini Nigeria kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Dkt Shein Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Nigeria nchini Dkt Sahabi Isa Gada,  ambaye alifuatana na wafanyabiashara na wawekezaji wa kampuni ya IBRU kutoka nchini humo.

Amesema Zanzibar ina rasilimali nyingi za uwekezaji hivyo ni vema wafanyabiashara na wawekezaji hao wakaangalia sekta wanazotaka na baadae kutumia fursa hiyo ya kuwekeza.

Kwa mujibu wa Dkt Shein, licha ya kampuni hiyo ya IBRU kuwa na uzoefu katika uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo ile ya uvuvi ambapo imeweza kuwekeza ndani na nje ya Nigeria, pia ni vyema wakaangalia uwezekano wa kuwekeza katika sekta nyingine zilizopo.