TANESCO yasisitiza mradi utakamilika kwa wakati

0
269

Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere katika bonde la mto Rufiji umefikia kwa asilimia 11 huku Shirika la Umeme nchini (TANESCO) likisisitiza kuwa utakamilika kwa wakati.

Katika kikao kazi maalum kilichofanyika jijini Dar es salaam kati ya Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu wakuu kutoka wizara mbalimbali pamoja na TANESCO, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt Tito Mwinuka amesema kuwa, wanasimamia kwa umakini mradi huo.

Mradi huo wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere utakapokamilika utaongeza ziada ya megawati elfu mbili mia moja kumi na tano za umeme katika gridi ya Taifa na kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa yenye umeme wa uhakika zaidi na ziada barani Afrika.

Kiongozi wa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu hao kutoka wizara mbalimbali Profesa Sifuni Mchome na Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati Zena Saidi wamesema kuwa mradi huo utaisaidia Tanzania kupata maendeleo makubwa zaidi.

Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere uliasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarsge Nyerere na unatekelezwa na serikali kwa gharama ya shilingi Trilioni 6.5.