Halmashauri zaagizwa kupunguza utitiri wa vikundi

0
323

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza halmashauri zote nchini kupunguza wingi wa vikundi vya akina mama, na badala yake watoe fedha kwa vikundi vikubwa ili kupata matokeo chanya na fedha hizo ziweze kurudishwa kwa wakati.

Makamu wa Rais amesema hayo jijini Dar es salaam katika kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya wanawake duniani na  miaka 25 baada ya mkutano wa Beijing.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, fedha zinazotolewa na halmashauri zimelenga kuwainua kiuchumi wanawake, vijana na wenye ulemavu na si kutumika kisiasa.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametumia kongamano hilo kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

Kauli mbiu ya kongamano hilo la kuadhimisha na kusherehekea siku ya wanawake duniani na  miaka 25 baada ya mkutano wa Beijing ni uwajibikaji wa uongozi katika kujenga kizazi cha usawa na jinsia.