Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa Kampuni ya Yapi Markez inayojenga reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR), Yetkin Genc Mehmet (54) amehukumiwa kulipa faini ya dola za Marekani (USD) milioni 100, sawa na shilingi bilioni 230.9 za Tanzania, ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani baada ya kukiri shtaka la kushindwa kutoa tamko la fedha USD 84,850, sawa na shilingi milioni 196, alizokutwa akizisafirisha.
Aidha mahakama imeamuru kutaifishwa kwa fedha hizo alizokutwa nazo Mehmet kuwa mali ya serikali.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesoma hukumu hiyo baada ya Mturuki huyo anayeishi Ilala, Dar es Salaam kufikishwa mahakamani Februari 27 na kusomewa shtaka moja la kushindwa kuzitolea taarifa fedha alizokutwa akisafiri nazo.
Mapema akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro amedai kuwa Februari 13, mwaka huu huko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (terminal III) mshtakiwa akiwa anaondoka nchini kwenda Instabul, Uturuki alikutwa na USD 84,850 ambazo hakuwa amezitolea taarifa kwa Idara ya Forodha.