City wapata ushindi wa kwanza Santiago Bernabeu

0
159

Manchester City wamepata ushindi wao wa kwanza kwenye dimba la Santiago Bernabeu kwa kuinyuka Real Madrid mabao mawili kwa moja katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Madrid ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo wakiwa na mataji 14, walitangulia kupata bao katika dakika ya 60 likifungwa na Isco Alceron na kisha kibao kikageuka kwa msako mkali uliowapa ushindi Man City kwa mabao ya Gabriel Jesus na Kevin De Bruyne.

Wakati huohuo nahodha wa Real Madrid, – Sergio Ramos ameonyeshwa kadi nyekundu ya nne katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya sawa na Edgar Davids na Zlatan Ibrahimovic ambao nao wamewahi kuonyeshwa kadi nyekundu mara nne katika  michuano hiyo.

Huko Groupama Stadium, -Cristiano Ronaldo ameshindwa kukibeba kibibi kizee cha Turin, -Juventus na kuambulia kichapo cha bao moja kwa nunge kutoka kwa Olympic Lyon ya Ufaransa.

Lucas Tousart aliipa uongozi wa mchezo wa kwanza Lyon kwa kuifungia bao pekee la ushindi katika dakika ya 31 huku akihitaji sare tu katika mchezo wa marudiano Machi 17 mwaka huu ili kutinga robo fainali.

Huu unakuwa ushindi wa kwanza kwa Lyon mbele ya Juventus katika mashindano ya vilabu Barani Ulaya, ambapo katika michezo minne waliyowahi kukutana Lyon alipoteza mara tatu na kuambulia sare mara moja.

Hata hivyo hii inakuwa mara ya kwanza kwa Juventus kupoteza mchezo dhidi ya timu ya Ufaransa tangu mwezi Novemba mwaka 2009 waliponyukwa mabao mawili kwa bila na Bourdeux wakati Lyon wao wakishinda mchezo wao wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwezi Februari mwaka 2012 walipoitandika Apoel Nicosia bao moja kwa bila.