Daktari mmoja nchini China amefariki dunia baada ya kuwatibu wagonjwa zaidi ya wagonjwa 3,000 walioathirika na virusi vya homa ya corona.
Liu Zhixiong aliyekuwa akifanyakazi katika hospitali moja katika Jimbo la Hubei nchini humo amefariki dunia kutokana na tatizo la shambulio la moyo baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya mwezi mmoja bila kupumzika, Global Times imeeleza.
Kifo chake kimeibua simanzi kubwa nchini humo, na taarifa zinaeleza kuwa hadi anafikwa na mauti hakuwa na maambukizi ya virusi hivyo hatari vya Corona.
Baadhi ya waliotoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wameshangazwa na kitendo cha kifo hicho kutokuripotiwa kuwa kimetokana na kazi, kwa maelezo kuwa uchovu alioupata ulitokana na kazi ya kuhudumia wagonjwa bila kupumzika.
Endapo kifo hicho kingeripotiwa kuwa kimetokana na kazi familia yake ingepaswa kulipwa fidia. Ingawa hakuna taarifa inayoelewa kwamba alilazimishwa kufanya kazi hiyo au alijitolea mwenyewe.
Kwa upande wake Serikali ya China imesema kuwa ina uhakika kwamba mlipuko wa virusi hivyo utakuwa umedhibitiwa ifikapo mwishoni mwa Aprili 2020.