Serikali kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano

0
327

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema serikali imekua ikitoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), lengo likiwa ni kujenga minara ya mawasiliano ili wananchi waweze kuwasiliana muda wote.

Mhandisi Nditiye ametoa kauli hiyo mkoani Lindi wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mavuji kilichopo wilayani Kilwa kabla ya kuzindua mnara wa mawasiliano uliojengwa na kampuni ya simu ya Tigo baada ya kupewa ruzuku na UCSAF.

Amesema mawasiliano hayachagui wala hayabagui, ndio maana serikali inahudumia wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa na kwamba serikali itahakikisha mawasiliano yanawafikia wananchi wote.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala ameishukuru serikali kwa kujenga mnara wa mawasiliano katika kijiji hicho na kuongeza kuwa kwa sasa wakazi wa kijiji hicho wanapata vizuri huduma za mawasiliano.

 “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli anasema CCM haichagui, haibagui. Mnara huu wa mawasiliano uliozinduliwa leo unatumiwa na watu wote wawe wanachama wa CCM, CUF, CHADEMA na chama chochote, huu ni utekelazaji wa sera za serikali na ilani ya CCM,” amesisitiza Bungala.