Jamii yatakiwa kupinga ukatili dhidi ya Wanawake

0
265

Jamii imetakiwa kuhakikisha inapinga ukatili wa aina zote, ili kufikia malengo ya kuwa na kizazi chenye usawa kati ya Wanawake na Wanaume.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Prudence Constantine amesema kuwa, kuelekea siku ya Wanawake Duniani machi Nane mwaka huu, kauli mbiu imelenga kutengeneza jamii yenye usawa kati ya mwanamke na mwanaume.

Amesema lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutathmini utekelezaji wa hatua za kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa katika kufikia maendeleo jumuishi.

Prudence amesema Serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuanzisha mfuko wa uwezeshaji kiuchumi na mfuko wa maendeleo ya wanawake ambao umesaidia kutoa mikopo nafuu na mafunzo ya stadi za biashara kwa wajasiriamali Wanawake.

Kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/2016 hadi 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 28.8 ambazo zimesaidia vikundi vya Wanawake 13,691 na kufanya idadi ya Wanawake wajasiriamali walionufaika na fedha hizo kufikia zaidi ya laki nane na elfu themanini ikilinganishwa na Wanawake 12,842 kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.