Lugola na wenzake kikaangoni

0
296

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekamilisha uchunguzi wa mkataba wa makubaliano kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini na kampuni ya ROM Solution LTD na kubaini kuwa mkataba huo ulikuwa ni batili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Februari 21, 2020, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa, mkataba huo ambao ungeliingizia Taifa hasara ya zaidi ya shilingi trilioni moja umebainika kuwa na makosa ya uhujumu uchumi.

Kufuatia hali hiyo,  Brigedia Jenerali Mbungo amesema TAKUKURU itapeleka jalada la mashtaka kwa mkurugenzi wa mashtaka kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Sakata la mkataba huo batili kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni ya ROM Solution LTD liliibuliwa na Rais John Magufuli Januari 23 mwaka huu na kupelekea kutenguliwa kwa uteuzi wa Kangi Lugola, aliyekua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa wakati huo, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Jacob Kingu kujiuzulu.

Mkataba huo ulikua ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.