Kumbukizi Vita vya Majimaji kufanyika Februari 22-27

0
270

Katika kuendelea kutunza na kuhifadhi urithi wa utamaduni nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Makumbusho ya Taifa wameandaa tamasha la Kumbukizi la Vita vya Maji Maji na tamasha la utalii wa utamaduni litakalofanyika mjini Songea.

Tamasha hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Baraza la Mila na Desturi la Mkoa wa Ruvuma pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) litaanza Februari 22 na kufikia mwisho Februari 27 mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Biseko Lwoga ameeleza baadhi ya malengo ya tamasha hilo ni pamoja na kutoa fursa kwa watanzania kuenzi, kutunza, kuendeleza urithi asilia, kuendeleza fursa za utalii wa utamaduni Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini kwa ujumla ili kuinua uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa eneo hilo.

“Urithi huu ni tunu na kioo cha Taifa la Tanzania na unaleta umoja, amani, na utangamano wa kitaifa ikiwa ni pamoja na kulitambulisha Taifa la Tanzania katika dunia ya sasa,”amesema Dkt Noel.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya maandalizi wa Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na tamasha la utalii mwaka huu, Christine Ngereza amesema watahakikisha wanahamasisha wananchi waweze kuanzisha makumbusho za jamii.

Siku ya kilele yatafanyika maandamano kutoka eneo waliponyongwa mashujaa 67 wa Vita vya Majimaji mpaka eneo la Majimaji yalipo makaburi ya pamoja ya mashujaa hao.

Kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Mchango wa Vita vya MajiMaji katika kuendeleza na kurithisha urithi wa utamaduni kwa maendeleo ya Taifa.”