Serikali kuajiri wafanyakazi wapya NIDA

0
457

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa wamebaini kuwa tatizo linaloisumbua Mamlaka ya Vitambulisho Tanzania (NIDA) ni upungufu wa wafanyakazi, lakini sasa serikali imejipanga kuongeza nguvu kazi ili wananchi zaidi waweze kuhudumiwa.

“Tumegundua kuwa NIDA ‘staffs’ (wafanyakazi) wake ni wachache mno, sasa tunaongeza watendaji wa NIDA, ili waweze kuwafikia wananchi.”

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Februari 21, 2020 wakati akizungumza katika mkutano na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani hapo.

Amesema kuwa licha ya kuwa muda wa mwisho wa kusajili laini kwa kutumia vitambulisho vya taifa ulishapita, lakini wananchi wasiwe na hofu kwani wote watapata vitambulisho hivyo na wataweza kusajili laini zao.

Aidha, waziri mkuu ametoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM mkoani Kigoma kutoa elimu kwa wakazi wa mkoa huo kuruhusu miradi ya maendeleo kupita kwenye maeneo yao ili waweze kunufaika nayo.

“Ukitaka eneo kwa ajili ya kujenga kitu kwa ajili ya manufaa yao, mpaka umlipe, sasa utalipa wangapi? Halmashauri inashindwa kufanya kazi yake, serikali inashindwa kufanya kazi yake, tena wakati mwingine watu hao sio watu wa kigoma,” amehitimisha waziri mkuu.