Stars yapangwa na Zambia, Namibia na Guinea michuano ya CHAN

0
533

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kwenye kundi D katika fainali za kuwania kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Cameroon mwaka huu.
 
Katika kundi hilo, Taifa Stars imepangwa na  timu za Taifa za Zambia, Namibia na Guinea.
 
Taifa Stars itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Zambia, mechi ya pili itakuwa dhidi ya Namibia na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi itacheza na Guinea.
 
Michezo yote hiyo ya hatua ya makundi ya Taifa Stars itachezwa kwenye mji wa Limbe wakati michezo ya kundi A itachezwa kwenye mji wa Younde na michezo ya kundi B na C itachezwa kwenye mji wa Duala.
 
Katika makundi mengine, kundia A linajumuisha wenyeji Cameroon, Mali, Burkina Faso na Zimbabwe.

Wakati kundi B lina timu za Libya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Congo Brazzaville na Niger huku kundi C likiwa na bingwa mtetezi Morocco, Rwanda, Togo na Uganda.
 
Fainali za CHAN kwa mwaka huu zitaanza kuunguruma Aprili Nne hadi 23 na hii ikiwa ni mara ya pili kwa Taifa Stars kucheza fainali hizo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 katika fainali zilizofanyika nchini Ivory Coast.