Wanandoa kuongezeka uzito, mitandao ya kijamii vyachangia kuongezeka talaka

0
543

Makanisa nchini Zambia yamewasihi wananchi kupunguza kasi ya matendo ambayo yanapelekea ndoa nyingi kuvunjika, ili kuwezesha watoto kupata malezi bora ya wazazi wote.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na gazeti la serikali ya Zambia, zaidi ya talaka 20,000 zilitolewa kwa wanandoa mwaka 2019 huku sababu ikiwa ni pamoja na tatizo la kuongezeka uzito kwa wanandoa.

Sababu nyingine zilizopelekea talaka hizo ni uasherati, ulevi, unyanyasaji wa kijinsia, tatizo la kupata ujauzito, matumizi ya mitandao ya kijamii, kushindwa kuhudumia familia, pamoja na ukosefu wa ushauri wa masuala ya ndoa kutoka kwa wataalmu.

Kiongozi wa MAkanisa ya Kujitegemea Zambia (Independent Churches of Zambia), Mwinjilisti David Msupa amesema kuwa takwimu hizo zinatisha na kusikitisha na kwamba zinakwenda kinyume na mpango wa dini unaoeleza kuwa kifo ndio kinapaswa kuwatenganisha wanandoa.

Takwimu zote zimeonesha kuwa wanawake ndio walioongoza kuomba talaka, huku umri wa watu ambao ndoa zao zimevunjika ukiwa kati ya miaka 25 hadi 45.

Mwinjilisti huyo amesisitiza kuwa makanisa yanatakiwa kuwasaidia wanandoa na kuwaeleza kuwa waasherati hawatourithi ufalme wa Mungu.