Ni miaka zaidi ya 120 tangu redio ilipoanza kutumika dunia, na mchango wake kwenye maendeleo ya jamii umeendelea kuonekana.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa ongezeko la vituo vya redio nchini, inaelezwa kuwa kumekua na tatizo la kuigana katika muundo wa vipindi, maudhui na hata mbinu za utangazaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Mhando amesema hayo jijini Dar es salaam wakati akifanya mahojiano na Waandishi wa habari kutoka Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kuhusu maendeleo ya redio nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani kwa mwaka huu.
“Wakati ule wa redio moja watu wengi walikuwa wanatusikiliza bila kuchoka, na siri moja iliyokuwepo ni ushindani ulikuwa miongoni mwetu watangazaji wa kituo kimoja, wakati hivi sasa ushindani upo miongoni mwa vituo vya redio,” ameeleza Mhando.
Ameongeza kuwa kikubwa kinachoharibu redio sasa hivi ni watangazaji kuigana sana badala ya kuwa wabunifu na mtangazaji mmoja kutaka kuwa kama mwingine.
“Si vibaya mtu ukamuiga mtu fulani ili kudokoa kitu, lakini ubaki wewe,” amehitimisha Tido.
Wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya redio duniani, Tanzania ina jumla ya vituo vya redio 204 ambapo kati ya hivyo, vituo 183 vinarusha matangazo katika masafa ya redio, na 21 ni redio za mtandaoni.