Madini yawanufaishe Watanzania – Profesa Idris Kikula

0
1718
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 12 Februari, 2020. Picha: Asher Thomas

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, amesema serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha madini yanawanufaisha watanzania na kukuza uchumi wa nchi.

Profesa Idris Kikula ametoa kauli hiyo katika nyakati tofauti kwenye ziara yake mkoani Njombe yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini.

Profesa Kikula amefafanua kuwa ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za madini, Serikali ilifanya maboresho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ili kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya uchumi wa madini kwa kujipatia kipato na kulipa kodi mbalimbali serikali.

MADINI: Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akitoa maelekezo kwa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu (katikati) katika eneo la Matarawe mkoani Njombe.                                                                                                       Picha: TBC/Asher Thomas

Kikula ameongea kuwa ili kuhakikisha huduma katika shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini zinaimarika, serikali imeongeza wataalam kwenye ofisi za madini na vitendea kazi kama vile,magari na mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Pia Profesa Kikula amewashauri wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwenye kampuni zinazojihusisha na utafiti na uchimbaji wa madini na kuunda vikundi vidogo vidogo ili kupewa leseni za madini na kuanza kuchimba mara moja.

KOKOTO: Shughuli za upondaji wa kokoto zikiendelea katika eneo la Matarawe mkoani Njombe.                                                                                           Picha: TBC/Asher Thomas

Profesa Kikula amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza mipango ya ufungaji wa migodi ili kuepusha athari za uharibifu wa mazingira zinazoweza kujitokeza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.

Vilevile amewataka wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria ya madini pamoja na kanuni zake.

MAZUNGUMZO: Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) kwenye machimbo ya kokoto ya Nyakamtwe mkoani Njombe.                                                 Picha: TBC/Asher Thomas

Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Profesa Kikula amesema ni pamoja na kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 serikali ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi Tsh 346 bilioni ikiwa imevuka lengo lililopangwa la kukusanya Tsh 310 bilioni.

Katika ziara yake kwenye machimbo ya madini, Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Njombe anayeshughulikia uchumi na uzalishaji, Gumbo Mvanda pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, na Tume ya Madini Makao Makuu.