Baadhi ya Watanzania walioko China wasema wako salama

0
559

Baadhi ya Watanzania wanaofanya kazi na kusoma nchini China wamesema kuwa, wako salama na wanapata huduma muhimu kama kawaida licha ya kuwepo kwa tishio la virusi vya Corona.

Wakizungumza kwa njia ya simu na TBC kutoka nchini China, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha South Central cha mjini Wuhan, Dkt Lyatamila Mtakwa na mwanafunzi wa chuo cha Poshan katika mji wa Guandong, Emilian Malya wamesema kuwa, kwa sasa bado wanaendelea kukaa ndani ili kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, lengo likiwa ni kujiepusha na maambukizi ya virusi vya Corona.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema kuwa, wamekuwa wakishirikiana na serikali ya nchi hiyo katika kuhakikisha wanatoa taarifa pamoja na mahitaji muhimu kwa Watanzania wanaoishi nchini humo.

Amewataka Watanzania wote waliopo China kufuata masharti yaliyowekwa ili kujikinga na virusi hivyo vya Corona.

Mpaka sasa, virusi vya Corona vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 1100, huku wengine zaidi ya elfu arobaini wakiugua homa ya virusi hivyo.