Sitoendelea na makongamano kwa sasa : Mwamposa

0
845

Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze Nabii na Mtume Boniface Mwamposa amesema kuwa, kwa sasa hatoendelea na makongamano aliyokuwa amepanga kufanya hadi hapo atakapotangaza tena.

Nabii na Mtume Mwamposa ametoa kauli hiyo mapema hii leo katika viwanja wa Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam wakati akielekea kuongoza ibada ya Jumapili ambayo amesema ni ya upako, ya kufunguliwa na kuponywa.

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni takribani wiki moja baada ya kutokea kwa tukio la vifo vya watu 20 na wengine 16 kujeruhiwa kwenye uwanja wa Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, katika kongamano lake la kukanyaga mafuta.

“Makongamano mengi nimeyasimamisha kwanza. Tunaomba neema ya Mungu ikapate kusimama na watu, na baada hapo ndipo nitaweka ratiba ya makongamano. Leo lilikuwa liwe kongamano kubwa la kukanyaga mafuta, kwa sababu ya shida iliyotokea tulisimamisha yote, tunataka utulivu na kumuomba Mungu atupe neema ya kupanga mipango mipya.” amesema Nabii na Mtume Mwamposa.

Ametoa pole kwa Watanzania wote kufuatia tukio hilo la Waumini kukanyagana na hatimaye kusababisha vifo na kuongeza kuwa anatambua kuwa tukio hilo limewaumiza Watu wengi pamoja na Serikali.

“Namuachia Mungu yeye mwenyewe asimame, kwa sababu lilikuwa jambo sio dogo, ni zito, limewaumiza Watanzania, serikali imeumia, viongozi wameumia lakini mengi tutayajua hapo mbeleni,” ameeleza Kiongozi huyo wa Kanisa la Inuka Uangaze.