Mfanyabiashara Godfrey Simbeye ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kuanzia Machi 31 mwaka huu.
Kaimu Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula ametoa taarifa kwa wajumbe, washirika, wahisani na umma kwa ujumla kuhusu uamuzi huo, huku akiwahakikishia wadau wote kwamba watahakikisha kipindi hiki cha mpito kinakuwa salama bila kuathiri utoaji wa huduma zao.
Katika taarifa hiyo ya Februari 7 mwaka huu Ngalula amemshukuru Simbeye kwa mchango wake mkubwa tangu alipojiunga kwenye taasisi hiyo, huku akimtakia heri katika masuala yake.
Hata hivyo sababu ya kiongozi huyo kung’atuka hazijawekwa wazi, lakini Ngalula amesema kwa Simbeye anataka kuelekeza muda wake katika shughuli nyingine.
TPSF imesema itatoa taarifa zaidi kuhusu mchakato wa bodi kutafuta kiongozi mwingine wa kuziba nafasi hiyo itakayoachwa na Simbeye baada ya kuitumikia kwa miaka 8.