Serikali imesema kuwa hadi Disemba mwaka 2019, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ulikuwa umekamilika kwa asilimia 70.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 jijini Dodoma Februari 7 mwaka huu.
Tanzania kuanza majaribio ya reli ya kisasa
Aidha, amesema kazi ya ujenzi kwa awamu ya pili ya SGR yenye urefu wa kilomita 422 kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma inaendelea vizuri.
Waziri Mkuu ametumia hotuba hiyo kueleza kuwa mbali na serikali kufanikiwa kurejesha matumizi ya treni ya abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro, bado jitihada zinafanywa reli hiyo iweze kufika mkoani Arusha.
Akielezea mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwamba serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa kwa lengo la kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara na reli katika maeneo yaliyoathirika na mvua zinarejea haraka.