Uturuki yachunguza ajali ya ndege iliyoua watu watatu

0
364

Serikali ya Uturuki inafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la ndege moja ya abiria ya nchi hiyo kuacha njia yake ya kurukia na kuingia kwenye majani,  hali iliyosababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Tukio hilo limetokea katika uwanja wa ndege wa Istanbul,  wakati ndege hiyo ya abiria ilipokuwa ikijaribu kutua.

Ndege hiyo ilikatika vipande viwili mara baada ya kutua kwenye uwanja huo huku ikiwa imeanza kuwaka moto.

Hali mbaya ya hewa inasemekana kuwa ni chanzo cha rubani wa ndege hiyo kuonekana kushindwa kuimudu alipokuwa akijaribu kutua.

Abiria na Wafanyakazi wa ndege hiyo walilazimika kuokolewa haraka kutoka katika ndege hiyo iliyokatika vipande viwili.

Abiria wengi waliokuwa ndani ya ndege hiyo ya Uturuki walitoka salama huku wakiwa na majeraha kidogo, ingawa baadhi walilazimika kupelekwa hospitalini.